UNICEF yawawezesha vijana kwenye kilimo nchini Kenya
12 September 2025

UNICEF yawawezesha vijana kwenye kilimo nchini Kenya

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Kaunti ya Kirinyaga, iliyoko katikati mwa nchi ya Kenya kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, inashuhudia mageuzi mapya katika sekta ya kilimo kupitia mradi wa kuwahusisha vijana  katika kilimo na lishe unaojulikana kama EKYAN. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, na wadau nchini humo.  Karibu Sabrina Saidi utupe taarifa zaidi.....(TAARIFA YA SABRINA SAIDI)Mradi wa EKYAN ni mfano wa ujasiriamali wa kilimo unaoongozwa na vijana, ukiwa na lengo la kutengeneza fursa za ajira, kuwanufaisha na kubadilisha maisha ya vijana walioko vijijini, kupitia mbinu bora za kilimo na lishe, ukitekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, serikali ya kaunti ya Kirinyaga na shirika linalotoa mafunzo, elimu ya biashara ndogo ndogo na uwezeshaji barani Afrika KUZA Biashara.Felista Nyakio Mutungi kijana mkulima wa kaunti ya Kirinyaga, ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo kupitia mradi huo. Na hapa anasema....CUT 2- Sauti ya Felista Nyakio Mutungi“Kabla ya kuanza kilimo, nilikuwa nauza barabarani viazi vya kukaanga au chipsi,  na mihogo, pamoja na nafaka. Haikuwa vizuri sana, lakini ndiyo nafasi pekee niliyokuwa nayo wakati huo. Kupitia serikali ya kaunti ya Kirinyaga, tulisajiliwa kama vijana wanaopenda kilimo na tukapata mafunzo kupitia KUZA na UNICEF. Sasa mimi ni mkulima na mjasiriamali.”Felista anasema awali alikuwa akilima robo ekari ya mpunga na kuvuna magunia manne hadi matano pekee. Lakini baada ya mradi wa EKYAN, kwa robo ekari hiyo hiyo sasa anapata hadi magunia saba. Aidha, shamba lake limepanuka hadi ekari nne katika eneo la 'mradi wa umwagiliaji wa Bura.Felista hakutaka kuwa mchoyo wa manufaa aliyopata, hivyo ameamua kueneza ujuzi wa kilimo cha kibiashara kwa kuwafundisha baadhi ya wakulima wengine mbinu na maarifa ya kilimo hiki.CUT- Sauti ya Felista  Nyakio Mutungi“Sasa si tu kwamba nalima, bali pia nawafundisha wakulima wengine kuongeza thamani katika mazao yao. Wanapata ujuzi wa kufanya biashara kupitia kilimo. Na kwa kweli tunawashukuru wahisani na UNICEF kwa kutuwezesha. Bila mpango huu, nisingekuwa hapa nilipo leo.”Kwa upande wake mtaalamu wa ubunifu wa UNICEF nchini Kenya Lilian Njoro, anaeleza kwa nini mradi huo ni muhimu kwa vijana.CUT- Sauti ya Lilian Njoro."Ni asilimia 10 pekee ya vijana wanaojihusisha na sekta ya kilimo. Kwa hivyo, kupitia mradi wa EKYAN, tulitaka kuona jinsi ya kuwahusisha vijana wengi zaidi katika kilimo na kuwavutia ili waweze kuanza kupata maisha yenye utulivu na ajira bora kupitia sekta hii.”Njoro anasisitiza kuwa teknolojia mpya zinafungua njia kwa kilimo cha kisasa tofauti na enzi za wazazi na mababu zao.Namna kilimo kinavyofanyika nyakati hizi ni tofauti na zamani,hii ni kwa sababu ya uwepo wa teknolojia bunifu, majukwaa ya kidijitali, na fursa nyingi.Kwa sasa, mradi wa EKYAN umeendelea kuwajengea vijana ujuzi, kuwapatia nafasi ya ajira, na kubadilisha mtazamo wao kuhusu kilimo, kutoka shughuli ya kizamani hadi kuwa biashara yenye faida.Link: https://youtu.be/hv17nk-2l5kTAGS:UNICEF Kenya/Kilimo/Biashara na ujasiriamali