Mshikamano wa nchi zinazoendelea kuchagiza SDGs
12 September 2025

Mshikamano wa nchi zinazoendelea kuchagiza SDGs

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Leo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea zikijulikana pia kama nchi za kusini ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa tamko lenye msukumo mkubwa likitambua ustahimilivu, ubunifu, na ushawishi unaoongezeka wa nchi zinazoendelea katika kuleta maendeleo ya kimataifa. Assumpta Massoi anatoa maelezo zaidi.(Taarifa ya Assumpta Massoi)Kwanza kabisa ni vema kufahamu kuwa nchi hizi zinaitwa za kusini, kwa maana kwamba bado ziko nyuma kimaendeleo zikilinganishwa na zile za kaskazini, (ingawa si kijiografia) ambazo zinaonekana kuwa zina maendeleo kiuchumi.Maudhui ya siku hii ni – fursa mpya na ubunifu kupitia ushirikiano wa kusini-kusini na ushirikiano wa pembetatu, ikimaanisha ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea, na vile vile mashirika ya kimataifa na nchi zilizoendelea.Sasa katika siku hii ya leo iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 22 mwezi Desemba mwaka 2003 kwa lengo la kusongesha ushirikiano wa kiufundi baina ya nchi zinazoendelea Guterres anasema “katika dunia inayozidi kuwa na nguvu nyingi za ushawishi, nchi zinazoendelea zinaonesha ustahimilivu wa kipekee na ubunifu wa hali ya juu. Sio tu katika kukabiliana na migogoro, bali pia katika kusukuma mbele mageuzi.”Mathalani nchi hizo zinabuni na kubadilishana majawabu bunifu katika maeneo muhimu kama vile kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, teknolojia rafiki kwa mazingira, fedha za kidijitali, na ubunifu katika sekta ya afya.Amesisitiza kuwa mafanikio haya yanajengwa juu ya misingi ya kuheshimu pande zote, kujifunza kwa pamoja, na lengo la pamoja—ambayo ndiyo misingi ya ushirikiano wa Kusini-Kusini na ule wa pembetatu.Hata hivyo amesisitiza kuwa ushirikiano huu si ishara tu ya mshikamano, bali pia ni nguvu kuu ya maendeleo inayohitajika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).Amepongeza juhudi za nchi za Kusini katika kuendeleza Ajenda ya 2030, licha ya changamoto zinazoendelea kama vile ukosefu wa usawa wa kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.Vilevile, ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutambua na kutekeleza wajibu wao katika kusaidia juhudi za maendeleo duniani.Katibu Mkuu anasema kuwa “tunatambua pia wajibu wa nchi zilizoendelea katika kushughulikia ukosefu wa usawa unaozidi kuongezeka na kuendeleza maendeleo endelevu.”Katika hitimisho la ujumbe wake, Guterres amehimiza jumuiya ya kimataifa kukumbatia ushirikiano wa nchi za kusini kama kichocheo cha kuhuisha ushirikiano wa kimataifa, akisisitiza haja ya kuchukua hatua kwa pamoja kujenga dunia iliyo jumuishi, yenye usawa, na endelevu kwa wote.Akizungumzia siku hii, , Mkurugenzi wa  Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya ushirikiano wa nchi za kusini, UNOSSC, Dima Khatib, amesisitiza kuwa nchi za Kusini zinamiliki "uwezo mkubwa wa kuendeleza maendeleo," kwani ndiko makazi ya asilimia 80 ya watu wote duniani na ni chanzo cha ustahimilivu, ubunifu, pamoja na rasilimali watu na asili ambazo hazijatumika kikamilifu.Katika mahojiano mahsusi na Idhaa ya  Umoja wa Mataifa, Bi. Khatib amesema kwamba katikati ya hali ya kisiasa ya kimataifa iliyojaa mvutano ambayo dunia inashuhudia leo, ushirikiano kati ya nchi za kusini unaweza kuwa injini ya kufufua na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.Amepigia chepuo ushirikiano kati ya nchi za kusini na zile za kaskazini akisema, “hakuwezi kuweko na mgawanyiok wa nchi kati ya zile za kaskazini zilizoendelea na zile za kusini zinazohaha kuendelea. Badala yake “lazima tujenge madaraja. Umoja wa Mataifa una uwezo wa kubeba jukumu hili kwa kuwa ni mfumo muhimu ambao unahudumia nchi zote kwa usawa.