Meli zilizokuwa zikipita Hormuz zilikuwa 129 kwa siku, sasa ni 2 hadi 7 kwa siku: UNCTAD
25 March 2026

Meli zilizokuwa zikipita Hormuz zilikuwa 129 kwa siku, sasa ni 2 hadi 7 kwa siku: UNCTAD

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Tangu kuanza kwa vita huko Mashariki ya Kati baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran mnamo tarehe 28 Februari na kisha Iran kujibu mashambulizi, wasiwasi umekuwa ukiongezeka kuhusu kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine. Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD linafuatilia kwa karibu hali inayoendelea na kutoa takwimu na uchambuzi ili kuzisaidia serikali na wadau wengine waweze kujipanga na kuratibu vyema mambo yao hususan yanayohusiana na usafiri wa baharini.Katikati ya vita hii inayoendelea Mashariki ya Kati kuna suala la mlango bahari wa Hormuz, hili ni eneo muhimu sana lililopo Iran ambako takriban robo ya mafuta yote duniani, meli zake hupita hapo. Bidhaa nyingine muhimu zinazopita hapo ni gesi asilia na mbolea. Ingawa mlango bahari wa Hormuz haujafungwa rasmi, lakini umewekewa vikwazo vikali, huku kukiwa na mashambulizi mengi ya Iran dhidi ya meli tangu vita vilipozuka siku 26 zilizopita. Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD Frida Youssef anaanza kwa kutueleza hali ilivyokuwa kabla ya vita.“Kabla tu ya mzozo, tunapoangalia wastani wa idadi ya meli kwa siku zilizokuwa zikipitia Hormuz, ilikuwa karibu meli 129, 130 na katika wiki mbili zilizopita, ilikuwa karibu meli mbili hadi saba kwa siku.”Kwa lugha nyingine upungufu ni takriban asilimia 95. Je ni maeneo gani yameathirika zaidi? “Usafirishaji wa mbolea unaathirika pamoja na bei ya uzalishaji, kwa mfano, mbolea za nitrojeni ambazo hutegemea sana gesi. Kwa hivyo, hii inabadilisha tena kuwa ni athari kwenye kilimo ambayo baadaye itaonekana kwenye kupanda kwa bei ya chakula.” UN News/Daniel DickinsonKufungwa kwa mlangobahari wa Hormuz kunaathiri biashara kwa kiwango cha kimataifa.Akiendea na tathmini yake Mkuu huyo wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi wa UNCTAD anasema hivi sasa bei za mafuta zimepanda.“Tumeona bei ya mafuta yanayotumika katika vyombo vya usafiri baharini ikiongezeka maradufu. Hii pia inaathiri gharama ya usafiri, si tu kwasababu bei ya mafuta imepanda bali pia bei, kwa mfano, ya bima. Malipo ya bima ya vita yameongezeka, katika baadhi ya maeneo imeongezeka mara nne.”UNCTAD inaendelea kufuatilia na kutoa taarifa kwa serikali na wadau kwani vita hii inayoendelea inaathari kwa kila mtu lakini nchi zenye uchumi mdogo ndio zitakazo athirika zaidi kwani zinauwezo mdogo zaidi wa kuvumilia mshtuko huu wa kiuchumi na ndio zitakazohisi athari zake kwa nguvu zaidi. “Inaathiri usafiri, inaathiri nishati, inaathiri chakula na pia inaongeza gharama na upatikanaji ni mgumu. Kwa hivyo, haya yote kwa pamoja yanakuwa na athari kwenye uchumi wa umma katika nchi, pamoja na gharama za maisha kwa kaya.”