Kwa mara ya kwanza watoto wenye utipwatipwa duniani ni wengi kuliko wenye utapiamlo
10 September 2025

Kwa mara ya kwanza watoto wenye utipwatipwa duniani ni wengi kuliko wenye utapiamlo

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Kwa mara ya kwanza idadi ya watoto na vijana wa umri wa kwenda shule wenye unene wa kupindukiaau utipwatipwa imezidi idadi ya watoto wenye utapiamlo duniani ikiathiri watoto milioni 188 sawa na mtoto 1 kati ya kila watoto 10 imesema leo ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Tuungane na Leah Mushi kusikia zaidi kuhusu ripoti hiyo, karibu LeahRipoti hii mpya ya UNICEF iitwayo “Faida kwenye vyakula: Jinsi Mazingira ya Chakula yanavyowaangusha watoto” imechambua takwimu kutoka nchi zaidi ya 190 na kubaini kwamba kiwango cha watoto wenye utapiamlo kimepungua tangu mwaka 2000, lakini wale wenye unene wa kupindukia kimeongezeka mara tatu.Kwa sasa, utipwatipwa umeenea katika kila eneo la dunia isipokuwa Afrika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini. Nchi za visiwa vidogo vya Pasifiki ndizo zinaongoza kwa kuwa na viwango vya juu zaidi, ikiwemo Niue yenye asilimia 38 ya watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 19 wakiwa na unene wa kupindukia.Nini kimesababisha?UNICEF inasema mabadiliko ya mifumo ya lishe kutoka vyakula vya asili hadi vyakula vya kutengenezwa kwa haraka na vya bei nafuu lakini vyenye sukari, mafuta na chumvi nyingi ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko hili.Pia inatahadharisha kuwa matangazo ya kidijitali ya vinywaji vyenye sukari na vyakula vya viwandani yanawafikia vijana wengi, hata katika nchi zenye migogoro.Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema utipwatipwa ni changamoto kubwa  ya kiafya kwa watoto kwa sababu huongeza hatari ya kupata kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo katika maisha ya baadaye.Russell amesema “Tunapozungumza kuhusu utapiamlo, hatuzungumzii tu kuhusu watoto wenye uzito mdogo, utipwatipwa ni changamoto kubwa inayoendelea kuongezeka ambayo inaweza kuathiri afya na maendeleo ya watoto. Vyakula vya viwandani vinazidi kuongezeka na kuchukua nafasi ya matunda, mboga mboga na protini katika wakati ambao lishe ina jukumu muhimu katika ukuaji wa watoto, ukuaji wa utambuzi na afya ya akili.”Nini kifanyike?Ili kukabiliana na hali hii, UNICEF inazitaka serikali kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kupiga marufuku uuzaji wa vyakula visivyo na lishe shuleni, kudhibiti matangazo ya vyakula vyenye sukari na mafuta, na kuweka sera za kusaidia familia kupata chakula bora na chenye lishe.Kwa mujibu wa UNICEF, bila hatua za haraka, gharama za kiafya na kiuchumi zitakazotokana na tatizo la utipwatipwa wa utotoni zinatarajiwa kupindukia dola trilioni 4 kila mwaka ifikapo mwaka 2035.Zipo juhudi za kupambana na hali hiyo ambazo zimeanza kuchukuliwa na baadhi ya nchi, mfano mzuri ni Mexico ambayo hivi karibuni imepiga marufuku uuzaji wa vyakula vilivyosindikwa na vile vyenye chumvi, sukari na mafuta mengi katika  maeneo ya shule za umma.