Harakati za UN na serikali ya Uganda kukabili tabianchi huko Karamoja
10 September 2025

Harakati za UN na serikali ya Uganda kukabili tabianchi huko Karamoja

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Karamoja, eneo la kaskazini mashariki mwa Uganda, linakabiliwa na changamoto kubwa za tabianchi kama vile ukame wa mara kwa mara na milipuko ya magonjwa ya mimea na mifugo, hali inayotishia uhakika wa chakula. Kupitia mradi wa PROACT, mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la  Chakula na Kilimo Duniani (FAO), na Mpango wa chakula Duniani (WFP) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya, EU, wameshirikiana katika kuimarisha mifumo ya kushughulikia mabadiliko ya kiikolojia na kijamii. Anold Kayanda na maelezo zaidi.(Taarifa ya Anold Kayanda) Video iliyoandaliwa na FAO inaanza ikionesha wana jamii katika eneo la Karamoja wanavyojihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kilimo na ufugaji licha ya changamoto za tabianchi.  Dustan Balaba Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Uganda anaeleza kuhusu mradi huu mpya akisema,"Wadau wameweza kuhakikisha kwamba kuna maendeleo ya haraka katika upatikanaji wa taarifa na tunatumia maendeleo ya kiteknolojia kwa manufaa yetu. Tumejiandaa vyema kutabiri matukio mengi ya tabianchi.”Mpango huu unalenga kutumia mifumo ya tahadhari ya mapema na hatua za kabla ya majanga ili kukuza uwezo wa jamii za Karamoja kukabiliana na majanga, pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kwa ushirikiano.Lokong Robert, Kaimu Afisa wa Kilimo wa Wilaya Kaabong anaeleza akisema, "Tunachagua kaya hizo. Baada ya kuchagua tunapewa maelezo juu ya madhumuni ya kuwachagua. viongozi wa meneo, maafisa wa ugani, na washauri wa ujenzi wa uwezo waliajiriwa na FAO huenda kukusanya taarifa katika kata."Naye Stella Nagujja, mtaalamu wa usimamizi wa hatari za tabianchi WFP Uganda anasema "mshikamano kati ya mamlaka zetu tofauti ulitufanya tufikiri kuwa itakuwa kimkakati kushirikiana na FAO ili kuokoa maisha na kuwafikia jamii zilizo katika mazingira magumu."Lakini kiini cha mradi huu kipo katika sauti za watu waliopokea huduma na kunufaika moja kwa moja. Kuanzia Moroto hadi Nabilatuk, jamii si wapokeaji tu wa msaada, bali ni washiriki  kamilifu katika kujenga uwezo wao wa kujitegemea.Jolly Aisu, afisa kilimo wilaya ya Nakapiripirit, anasema ,  “tunapanga ziara za mashambani ili kutusaidia kutambua na kuchambua ugonjwa au mdudu gani ameshambulia mimea ya mkulima. Kisha kutoka hapo tunawaelekeza cha kufanya kutumia taarifa kutoka katika mifumo ya tahadhari ya mapema na mipango iliyo wazi.”Hata hivyo, pamoja na maendeleo haya, changamoto bado zipo. Rasilimali chache na hali ya ukosefu wa usalama miongoni mwa jamii vinaweza kuhatarisha mafanikio ya mradi huu.Lukeng  Emmanuel, Mkulima wa Kaabong anatamatisha kwa kusema, "Tunashindwa hata kununua dawa ya kunyunyizia kwa sababu kile kidogo tunachokipata hapa tunatumia kwa chakula, karo ya shule, na matibabu. Tunaliacha shamba lipambane kivyake hadi tutakapopata pesa kidogo ya kununua dawa ndipo tunanyunyizia."