Furaha ni pale ninapoweza kuhudumia familia yangu
23 March 2026

Furaha ni pale ninapoweza kuhudumia familia yangu

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Furaha ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 20 Machi, wakazi wa kata ya Luchelele, jijini Mwanza, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, wameeleza maana ya furaha katika maisha yao ya kila siku, ambapo kwa wengi, furaha haitokani na anasa, bali inajengwa na afya njema, upendo wa familia, na uwezo wa kuitunza familia hiyo kwa mahitaji ya msingi. Wakizungumza na Rashid Malekela wa Idhaa hii, wanawake wa eneo hilo wameeleza kuwa furaha kwao ni chanzo kikuu cha amani ya moyo. Rehema James amesema kuwa furaha yake kubwa ni kuamka salama, wakati Regina Emmanuel amegusia uhusiano wa mzazi na mtoto kama nguzo ya furaha yake, "Furaha yangu kuu inatokana na mama yangu kuwa hai na mwenye afya."Faida Anthony, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amefafanua kuwa kwake furaha ni matokeo ya jitihada za kutafuta riziki akisema,"Furaha ni kutafuta fedha, mboga, na kuijali familia yangu."Mitandao ya kijamii na changamoto za furahaLicha ya umuhimu wa afya na familia, matumizi ya teknolojia yameanza kuathiri jinsi watu wanavyopata au kupoteza furaha katika ulimwengu wa sasa. Duch Sababu, ambaye ni Afisa Usafirishaji maarufu ‘bodaboda’, amebainisha kuwa mitandao ya kijamii ina sura mbili; inaweza kuleta kicheko kupitia maudhui ya ucheshi au kuleta huzuni kulingana na kile mtu anachokiona, huku akitoa angalizo kwa watumiaji wa mitandao,"Furaha ni afya njema, lakini pia mitandao inaweza kuleta furaha kupitia vichekesho au huzuni kulingana na kile unachokiona."Wito wa Umoja wa MataifaMwaka huu, Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa furaha ya kweli kwa binadamu wote itafikiwa endapo kutakuwa na usawa, haki, na ulinzi wa mazingira kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Ili kufikia malengo hayo duniani, kuna uhitaji wa kuendelea kuimarisha huduma za kijamii zinazogusa maisha ya watu wa hali ya chini moja kwa moja.Kwa vijana, wameshauriwa kutumia muda wao kwenye mitandao ya kijamii kutafuta mambo yatakayowajenga kifikra na kuwapa furaha badala ya mambo yanayoweza kuwaharibia amani yao ya moyo.