Skip to content
Opens in a new window
About
Hii leo tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya, katika Kijiji cha Embulbul kilichoko Kaunti ya Kajiado, ambako Shirika lisilo la kiserikali la Tulivu Safe Haven, lililoanzishwa kwa kushirikiana na wadau wakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa, linatekeleza hatua mbalimbali za kuwasaidia wanawake. Hii ni pamoja na kuwaokoa na kuwahifadhi manusura wa ukatili wa kijinsia kwa kuwapatia makazi salama, ushauri nasaha, msaada wa kisheria na uwezeshaji wa kiuchumi, sambamba na kuwarejesha shuleni wasichana walionusurika. Je, nini kinafanyika? Kupitia video iliyoandaliwa na Redio washirika wetu Domus, Feissal Kirwa amefuatilia simulizi za manusura na kutuandalia makala hii. Pia tunakuletea muhtasari wa habari.Maabara tembezi ya kupima virusi vya Ebola imewekwa katika mji wa mpakani wa Kasenyi ulioko kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako kuna hatari kubwa ya kushamiri kwa mlipuko wa Ebola kutokana na harakati nyingi za safari. Dkt. Olga Ntumba kutoka WHO ambayo inafadhili maabara hiyo inayotoa majibu ndani ya saa moja, amesema “virusi haviheshimu mipaka. Maabara hii ina mchango muhimu kubaini mapema wagonjwa, kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa, kubadilishana taarifa na juhudi za mwitikio kwenye ukanda mzima.”Mioto ya nyika ikiendelea kutikisa maeneo ya kaskazini mwa dunia shirika la Umoja wa Matiafa la Afya duniani, WHO limekumbusha kuwa moshi utokanao na mioto hiyo ya nyika huvuka taifa, kanda na hata mabara na kuwa na madhara kwa watu hata wanaoishi mbali na moto wenyewe. Hivyo limetangaza mambo tisa ya kuzingatiwa ikiwemo kusikiliza taarifa za mamlaka kama vile viwango vya uchafuzi wa hewa, kuvaa barakoa na kusalia ndani ya nyumba na kufunga madirisha iwapo hujashauriwa kuhama.Na wiki ya kimataifa ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama ikianza kesho Agosti Mosi, Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake, lile la afya, (WHO) na la kuhudumia watoto, (UNICEF) umetaka nchi kuimarisha mifumo ya afya ili iweze kupatia akina mama na watoto wachanga msaada wa kufanikisha unyonyeshaji bora ambao ni msingi wa ukuaji bora wa mtoto na afya ya mama anayenyonyesha. Halikadhalika utekelezaji wa kanuni ya kimataifa kuhusu matangazo ya bidhaa za mbadala wa maziwa ya mama.Mwenyeji wako ni Anold Kyanda, karibu!