Skip to content
Opens in a new window
About
Hii leo tunakuletea mada kwa kina. Mlipuko wa sasa wa ebola ya virusi vya Bundibugyo uliotangazwa rasmi huko DRC mwezi Mei mwaka huu unazidi kuongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida, wamesema maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wakizungumza na waandishi wa habari Karl Skau, Kaimu Mkuu wa WFP, na ndio tunakupeleka nchini humo kufuatilia juhudi za kuudhibiti.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema ni wakati wa dunia kuungana kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa watu, hususan aina mpya inayokua kwa kasi ya kulazimishwa kufanya utapeli kwa njia ya mtandao. Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Watu inayoadhimishwa kila mwaka tarehe thelathini Julai, amesema wahalifu wanawavutia watu kwa ahadi za ajira nzuri, lakini baadaye wanawafanya mateka na kuwalazimisha kuendesha utapeli mtandaoni. Guterres amezitaka nchi kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Uhalifu wa Mtandao uliopitishwa mwaka 2024, kushirikiana kuvunja mitandao ya uhalifu na kuwasaidia manusura kurejea katika maisha yao ya kawaida.Nchini Ukraine, mashambulizi makubwa ya usiku yaliyojumuisha makombora na mamia ya ndege zisizo na rubani yamesababisha vifo na majeruhi katika maeneo kadhaa ya makazi, yakiwemo miji ya Kryvyi Rih, Kyiv na Lviv. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA, imesema nyumba na shule za awali zimeharibiwa huku watoto wakiwa miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa. Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema watoto watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku likiendelea kutoa msaada wa dharura wa kisaikolojia na usaidizi wa kifedha kwa familia zilizoathirika.Na Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amelaani hatua za serikali ya Uganda zinazodaiwa kuendelea kubana uhuru wa msingi na kuzima sauti za wanaokosoa serikali. Amesema tangu uchaguzi mkuu wa Januari mwaka huu, viongozi wa upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari wamekumbwa na vitendo vya kutoweshwa, kukamatwa kiholela na mateso. Kupitia taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Bwana Türk ni kwamba ofisi hiyo imepokea taarifa zinazoonesha kuongezeka kwa ushiriki wa jeshi katika kutekeleza majukumu ambayo kwa kawaida hufanywa na taasisi za kiraia. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari vimelazimika kusitisha shughuli zake kwa muda.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, na leo tunamkaribisha Ntahombaye Hussein, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Kiswahili nchini Burundi, CHAWARUNDI. Anafafanua maana ya neno, “KUSOROZA. ”Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!