Skip to content
Opens in a new window
25 SEPTEMBA 2026
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa leo unafanyika mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu maandalizi dhidi ya majanga ya milipuko ya magonjwa na kama nilivyokudokeza kuwa tutakuwa na maoni na ushauri wa baadhi ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa viongozi wanaoshiriki mkutano huo, tunaanzia nchini Uganda, kisha tuelekee nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Pia tunakuletea muhtasari wa habari.

• Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo linafanya Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Kuzuia, Kujiandaa na Kukabiliana na Magonjwa ya Milipuko, unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kupitisha tamko la kisiasa kuhusu maandalizi na mwitikio wa magonjwa ya milipuko. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres, Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed amesema dunia inahitaji mshikamano, usawa na hatua madhubuti za kimataifa ili kutomwacha mtu yeyote nyuma na kujifunza kutokana na uzoefu wa hivi karibuni akisema “Janga la COVID-19 lilitufundisha kwamba, katika dunia yetu iliyounganishwa, hakuna nchi inayoweza kujilinda yenyewe. Tulijifunza jambo hili kwa gharama kubwa sana ya kibinadamu na kiuchumi.”
• Tukielekea Afrika, Hama hama ya watu kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, inmelilazimu Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, kuongeza ufuatiliaji wa Ebola katika mipaka, vituo vya wakimbizi na njia za usafiri. Hadi Septemba 21, zaidi ya watu 7,700 walikuwa wamethibitishwa kuwa na Ebola, huku 3,700 wakifariki.
• Na nchini Yemen takriban watoto milioni 2.2 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakumbwa na utapiamlo kila uchao hawajui pa kula wala pa kulala kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likisistiza kuwa usalama ndio kipaumbele ili watoto hao waweze kuishi kama Watoto. Akizungumza Geneva Uswisi kwa njia ya video kutoka Aden, Yemen Mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Akhil Iyer, amesema “Tunashuhudia ongezeko la utapiamlo mkali mtoto 1 kati ya 4 anautapiamlo mkali na Watoto 200 wako katika hali mbaya sana ya unyafuzi.”
Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!