About
Hii leo jaridani tunaangazia usalama wa mabaharia katika Mlango Bahari wa Hormuz, ongezeko kubwa la ukatili wa kingono unaohusiana na mzozo nchini Sudan, na ujumbe wa Papa Leo wa Kumi na Nne (Leo XIV), kuhusu ongezeko la njaa duniani.Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) limetangaza mpango wa kuwaondoa zaidi ya mabaharia 11,000 waliokwama katika Mlango Bahari wa Hormuz kufuatia makubaliano ya amani kati ya Iran na Marekani yaliyolenga kurejesha usalama wa usafiri wa baharini katika eneo hilo. Anold Kayanda amefuatilia hatua hiyo.Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR, imetoa ripoti kuhusu ongezeko kubwa la ukatili wa kingono unaohusiana na mzozo nchini Sudan tangu mapigano yalipoanza zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Ofisi hiyo imekumbusha jumuiya ya kimataifa umuhimu wa kuhakikisha haki na uwajibikaji vinapewa kipaumbele wakati juhudi za kusitisha mapigano na kutafuta suluhu ya mzozo huo zikiendelea.Katika kipindi ambacho idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani inaendelea kuongezeka kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo wa Kumi na Nne (Leo XIV), ametuma ujumbe wa mshikamano kwa kutembelea makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, mjini Roma nchini Italia wiki hii. Ziara hiyo imeangazia umuhimu wa kuimarisha juhudi za kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!