
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoturejesha hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo Leah Mushi ameketi chini na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nassriya Nassir Ali akieleza safari yake ya uongozi wa nafasi za umma kupitia mkalimani wake wa lugha ya alama Tusajigwa Ernest. Pia tunakuletea Muhtasariw a habari na jifunze Kiswahili.Janga la tabianchi linakaribia kwa kasi zaidi kuliko inavyodhaniwa ameonya leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, huku akitoa wito wa hatua saba za haraka kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuachana na matumizi ya mafuta ya kisukuku. Akizungumza mjini London kwenye mkutano wa hatua dhidi ya tabianchi, ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na Serikali zichukue hatua madhubuti za tabianchi, dunia iongeze matumizi ya nishati safi, ilinde jamii zilizo hatarini, ihakikishe ufadhili wa haki kwa nchi zinazoendelea, isimamie kwa uwajibikaji matumizi ya teknolojia ya akili mnemba na kupambana na upotoshaji wa taarifa kuhusu tabianchi. Guterres amesema hatua hizo ni muhimu ili kudhibiti ongezeko la joto duniani na kuzuia madhara makubwa zaidi kwa binadamu na mazingira.Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, limekaribisha makubaliano mapya kati ya DRC na Rwanda ya kusaidia wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari, usalama na heshima. Katika mkutano uliofanyika Addis Ababa Ethiopia, serikali za nchi hizo mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwa msaada wa UNHCR ili kuwezesha urejeaji salama wa wakimbizi.Zaidi ya wagonjwa 1,000 vya Ebola wamethibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, huku watu 254 wakifariki dunia kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO likiongeza kuwa wagonjwa 100 wamepona, jambo linaloonesha kuwa huduma ya afya ya haraka inaweza kuokoa maisha.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana za neno "TANUWINI"Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!