About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI, UNAIDS kupitia ripoti yake mpya limeonya kuwa kupungua kwa ufadhili wa kimataifa na uwekezaji mdogo katika huduma za kinga dhidi ya Virusi vya UKIMWI, VVU kunaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya UKIMWI duniani.Katika hatua za mwitikio wa kitaifa, wiki iliyopita, Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania, TACAIDS kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini humo imeendesha warsha ya siku tano kuanzia Juni 15 hadi 19 kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wa asasi za vijana na wawakilishi wa vijana katika utetezi wa masuala ya VVU na Afya ya Uzazi. Pia tunakuletea Muhtasariw a habari.Leo katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, viongozi wa dunia wanakutana katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Virusi vya UKIMWI VVU, na UKIMWI kujadili mafanikio na changamoto za mapambano dhidi ya janga hilo tangu mwaka 2021. Mkutano huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano unalenga kupitisha Azimio jipya la Kisiasa litakaloelekeza hatua za dunia katika kukabiliana na UKIMWI kwa miaka mitano ijayo.Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women, limeonya kuwa matumizi ya akili mnemba au AI yanaongeza hatari ya ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana duniani. Utafiti wa mifumo 133 ya AI umebaini kwamba asilimia 44 ilikuwa na upendeleo wa kijinsia, huku asilimia 26 ikiwa na ubaguzi wa kijinsia na rangi kwa pamoja.Na Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, hatua za kujikinga dhidi ya Ebola zimeimarishwa katika Gereza Kuu la Bunia ambako zaidi ya wafungwa 2,000 wanaishi katika mazingira ya msongamano mkubwa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO kanda ya Afrika, kwa ushirikiano na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, wamejenga kituo maalum cha muda cha kutenga wagonjwa wa Ebola.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!