Skip to content
Opens in a new window
21 OKTOBA 2026
About
Hii leo jaridani tunakuletea Mada kwa Kina. Kwa vijana wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, wakimbizi na wale wanaorejea katika jamii baada ya kutoka gerezani, kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia kujenga maisha yao ni jambo muhimu.

Mradi wa Lens on Life ulioanzishwa mwaka 2016 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, unatumia sanaa ya upigaji picha kuwapa vijana ujuzi wa kisanii na fursa za kujipatia kipato. Cynthia Akhangwa wa Idhaa hii amezungumza na Jack Powers, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa mradi huo, alipokutana naye katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili:

• Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) limeendelea kusisitiza kuwa hakuna sababu ya vikwazo vya biashara, safari au mikusanyiko ya umma wakati huu ambapo Nigeria imekuwa nchi ya 5 kuthibitisha kuwa na mgonjwa wa Ebola ya Bundibugyo, aliyeingia nchini humo akitokea Uganda hivi karibuni, akaugua tarehe 7 Oktoba na jana Oktoba 20 kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo. Mgonjwa yuko kwenye matibabu na waambata wake wanafuatiliwa. Nayo Kenya leo imeripoti mgonjwa wa 9, naye ni miongoni mwa waambata wa mgonjwa wa kwanza aliyefariki dunia Oktoba 5, na tayari aliikuwa kwenye karantini.
• Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa ya pengo la uzalishaji wa hewa chafuzi imetolewa leo ikisema kuwa kiwango cha ongezeko la joto duniani kinatarajiwa kuzidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyaji, juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, hivyo upunguzaji wa haraka na mkali wa uzalishaji wa gesi chafuzi unahitajika ili kupunguza muda wa kuvuka kikomo hicho. Akizungumzia hali hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “lakini kuvuka kiwango hicho cha ongezeko la joto si kusalimu amri. Bado tunaweza kuhakikisha kwamba ongezeko hilo linabaki kuwa dogo na la muda mfupi iwezekanavyo, na kurudisha viwango vya joto chini ya nyuzi joto 1.5 kabla ya mwisho wa karne hii. Pengo la kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi sasa limekuwa pengo la uongozi. Na dunia inazidiwa na wakati na visingizio vya kuliziba pengo hilo
• Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya Hewa, (WMO) limeonya kuwa El Niño inayotarajiwa baadaye mwaka huu huenda ikawa miongoni mwa El Nino lenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 40, hali inayotarajiwa kusababisha mabadiliko makubwa ya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali duniani. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tathmini mpya ya tabianchi ya msimu, Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, amesema kiwango cha joto kwenye uso wa bahari katika eneo la bahari ya Pasifiki ukanda wa kitropiki ambalo ndio kitovu cha El Niño, linaweza kufikia nyuzi joto 3.8 katika kipimo cha Selsiyasi, ikiwa ni juu ya wastani kati ya Novemba 2026 na Januari 2027
• Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno "MAFINGU"
Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!