
About
Hii leo jaridani tunaangazia wito wa UN wa kulinda mamilioni wa wakimbizi kote duniani, masuala ya kijinsia Zanzibar nchini Tanzania, na ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu watoto katika maeneo ya machafuko imeonesha hali ya kutisha duniani.Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakimbizi kesho Juni 20, viongozi wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuimarishwa kwa mshikamano na hatua za kimataifa za kuwalinda mamilioni ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kote duniani kutokana na vita, vurugu na mateso.Ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika maeneo ya machafuko imeonesha hali ya kutisha duniani. Takribani watoto 24,174 waliuawa, kujeruhiwa, kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha, kubakwa au kuathiriwa kwa namna nyingine na ukiukwaji mkubwa wa haki katika maeneo yenye mizozo mwaka 2025.Je, maisha yangekuwaje kama kila manusura wa ukatili wa kijinsia angejua mahali pa kupata msaada kwa wakati? Kisiwani Zanzibar nchini Tanzania Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women), kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU) na kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, linaimarisha upatikanaji wa haki na huduma za msaada kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, hususan katika maeneo ya pembezoni. Kupitia mradi wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana Zanzibar na Kuimarisha Uongozi wa Wanawake, manusura wanapata habari muhimu, ushauri nasaha na msaada wa kisheria wakati wowote.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!