
About
Hii leo jaridani tunaangazia masuala ya Akili Mnemba na wabunifu wa maudhui duniani kwa lugha, waumini wa dini ya kiislamu wakati huu wa Ramadhani katika ukanda wa Gaza, na matibabu ya kwanza ya ugonjwa wa kichocho huko Mwanza nchini Tanzania.Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema wabunifu wa maudhui duniani kwa lugha ya kiingereza content creators wanakabiliwa na hatari ya kupoteza hadi asilimia 24 ya mapato yao ifikapo mwaka 2028 kutokana na kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba, au AI.Waumini wa dini ya kiislamu duniani kote wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kipindi kinachoambatana na sio tu ibada bali pia mlo kama vile futari na daku. Hata hivyo kwa wakazi wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na kimabavu na Israeli hali si hali kwani mlo na mengine yanayoambatana na kipindi hiki vinasalia kuwa ndoto.Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP kupitia Ushirikiano wa Upatikanaji na Ufikishaji wa Huduma (ADP), inaendesha mpango wa majaribio wa kihistoria katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, na Kigoma ili kutoa matibabu ya kwanza ya ugonjwa wa kichocho yaliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.Mwenyeji wako ni Anold Kyanda, karibu!