18 DESEMBA 2025
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ya vijana wanaotafuta fursa za mafunzo kwa vitendo. Umoja wa Mataifa ni moja ya mashirika ya kimataifa yanayotoa fursa hii kwa vijana kutoka duniani kote kuja hapa Makao Makuu jijini New York Marekani au hata katika nchi husika.Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imefichua mauaji ya kutisha, ubakaji na matumizi ya njaa kama silaha ya vita katika kambi ya Zamzam, Darfur, Sudan. Kwa mujibu wa ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, raia wasiopungua 1,013 waliuawa katika mashambulizi ya siku tatu ya wanamgambo wa RSF mwezi Aprili, huku zaidi ya watu 400,000 wakilazimika kukimbia makazi yao.Leo, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemulika mchango mkubwa wa mamilioni ya wahamiaji duniani, wakati uhamiaji ukiendelea kuwa mgumu zaidi kutokana na migogoro, majanga yanayohusiana na tabianchi na shinikizo za kiuchumi. Ameeleza kuwepo kwa viwango vya juu zaidi vya watu waliolazimika kuhama makazi yao na idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa ya vifo vya wahamiaji wakiwa safarini, huku akisisitiza kuwa uhamiaji salama na unaosimamiwa vyema unaweza kuchochea ukuaji wa uchumi, ubunifu na maendeleo katika nchi za asili na zinazopokea wahamiaji. Guterres amesema, “Uhamiaji unapokuwa salama na unasimamiwa vyema, si janga la kuogopa, bali ni nguvu kubwa ya kuleta mema.”.Na Ama K. Babebrese Balozi mwema wa kitaifa wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM mwenye asili ya Ghana ambaye sasa ni muhamiaji nchini Uingereza, katika siku hii ya uhamiaji ametoa ujumbe maalum akisema "Napenda kumtia moyo kila mtu kwamba tunaweza kuwa tofauti, hadithi zetu za uhamiaji ni tofauti tumetoka kwenye mazingira tofauti lakini kitu cha muhimu ni kwamba kama jamii sisi ni kitu kimoja. Uhamiaji ndio hadithi yangu”.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!