
About
Hii leo jaridani tunaangazia ripoti ya UNDP ya umaskini, mradi wa kusaidia jamii kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Zambia na juhudi za kuboresha hali ya lishe kwa watoto nchini Kenya.Takribani watu milioni 887 duniani ambao ni maskini wanaishi kwenye maeneo yanayokumbwa moja kwa moja na madhara manne yasababishwayo na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni joto kali, mafuriko, ukame na uchafuzi wa hewa, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP kwa kushirikiana na wadau. Ripoti inaonesha bayana kuwa hali hiyo inazidi kutwamisha watu hao kwenye hali tete zaidi.Mradi wa kusaidia jamii kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Zambia mbali na kusaidia wananchi kwenye kilimo pia umewawezesha kiuchumi na kuwaondoa baadhi yao kwenye mstari wa umasikini. Mmoja wa walio utupa mkono umasikini ni Judith Mabeta aliyetoka kuishi nyumba ya udongo mpaka kuwa na nyumba ya kupangisha na sasa ni mama mwenye nyumba.Kupitia msaada wa fedha kutoka Ufaransa, juhudi za kuboresha hali ya lishe kwa watoto nchini Kenya, hasa kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi zinaendelea ambapo juhudi za hivi karibuni ni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya ambao kwa pamoja wameimarisha huduma hizo kwa manusura wa mafuriko Magharibi mwa taifa hilo la Afrika Mashariki. Huduma hizi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha watoto na familia wanapata vyakula vyenye virutubishi kwa ustawi wa maisha yao.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!