
About
Hii leo jaridani tunaangazia ripoti ya mauaji wa wanawake na wasichana Gaza, ukatili wa kijinsia na wa kingono unaotumiwa kama silaha ya vita Sudan, na msaada wa dawa na matibabu ya bure nchini DRC yanyoendeshwa na walinda amani wa MONUSCO kutoka Tanzania.Uchambuzi mpya wa utafiti uliotolewa leo Aprili 17 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN Women umeweka wazi kuwa zaidi ya wanawake na wasichana 38,000 wameauawa kati ya mwezi Oktoba mwaka 2023 na Desemba 2025 huko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel ikiwa ni wastani wa takribani wanawake na wasichana 47 wanaouawa kila siku. Anold Kayanda ameufuatilia utafiti huo na kutuandalia taarifa ifuatayo.Ukatili wa kijinsia na wa kingono unatumiwa kama silaha ya vita nchini Sudan, jambo ambalo limesahaulika huku migogoro ikiendelea katika maeneo mengi mengi kote duniani amesema Tonderai Chikuhwa, Mshauri Mwandamizi wa Sera katika Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Ukatili wa kijinsia katika Migogoro, katika mahojiano na Khaled Mohamed wa Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa.Raia wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, waishio mji wa Oicha uliopo Mavivi katika Jimbo la Kivu Kaskazini, wamewashukuru walinda amani kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa Kikundi cha Tano Cha Utayari (TANZQRF-05), kinachohudumu chini ya mwamvuli wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani nchini humo (MONUSCO) kwa kutoa msaada wa dawa na huduma za kitabibu kwenye Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mji wa Oicha wiki hii.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!