
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Uganda ambayo ni moja ya nchi zinazohifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani na tutasikia simulizi za wakimbizi kutoka Sudan ambao Uganda iliwapokea na kuwapa makazi katika Makazi ya Wakimbizi ya Kiryandongo yaliyoko magharibi mwa nchi.Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametaka uchunguzi wa haraka na uwajibikaji wa kimataifa kufuatia madai ya usafirishaji haramu wa wanawake na wasichana yaliyoibuliwa katika “faili za Epstein.” Wamesema madai hayo yanaonyesha mtandao mpana wa unyonyaji wa kingono uliodumu kwa miaka mingi na kuhusisha watu mashuhuri.mashambulizi makali ya anga ya Israel yameendelea kusini mwa Lebanon, yakilenga maeneo karibu na ngome ya Hezbollah ya Bint Jbeil, huku mashambulizi ya roketi kuelekea kaskazini mwa Israel nayo yakiendelea na kuongeza hofu ya kuongezeka kwa mapigano. Katika hatua nyingine, jeshi la Marekani limesema limezuia meli 10 kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz, likitekeleza zuio lake lililotangazwa dhidi ya bandari za Iran. Wakati huo huo, mvutano wa kidiplomasia unaongezeka katika Umoja wa Mataifa, ambapo Baraza Kuu linakutana leo kujadili matumizi ya kura ya turufu kufuatia azimio la Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati lililoungwa mkono na wengi lakini kuzuiwa na China na Urusi.Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, leo limeeleza wasiwasi mkubwa kufuatia ongezeko la watoto waliouawa au kujeruhiwa nchini Ukraine, ambapo watoto 89 wameathirika mwezi Machi 2026 pekee. Kwa mujibu wa takwimu zilizothibitishwa na ripoti ya uangalizi wa haki za binadamu nchini Ukraine, idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 65 ikilinganishwa na mwezi Februari, hali inayoonesha madhara makubwa ya mashambulizi yanayoendelea kwa familia na jamii. Mashambulizi mabaya ya usiku wa tarehe 15 Aprili yalipiga miji kadhaa mikubwa, ikiwemo Dnipro, Kharkiv, Kyiv na Odesa, yakionesha hatari kubwa inayowakabili watoto.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye Kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “AWALI KUWA HERI SI AJABU” asMwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!