Skip to content
Opens in a new window
15 OKTOBA 2026
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa. Mwezi uliopita wa Septemba, huko jijini Nairobi nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO) kwa kushirikiana na serikali ya Kenya na wadau wengine walizindua mradi wa SoilFer.

Pamoja na mambo mengine, mradi huu una lengo la kuhakikisha wakulima wanapata tija kupitia udongo wenye afya. Stella Vuzo kutoka Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa nchini Kenya alikuwa shuhuda wetu na alizungumza na wadau mbali mbali hasa kuhusu hoja ya afya ya udongo.

Pia tunakuletea muhtasari wa habari:

• Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO nchini Kenya, Dkt. Neema Kimambo amezungmza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya na kusema mgonjwa wa pili wa Ebola ya virusi vya Bundibubyo aliyethibitishwa na serikali jana Jumatano sasa anapatiwa matibabu na kwamba, “mgonjwa huyu ni ndugu wa yule mgonjwa wa kwanza na ulikutana na yule mgonjwa alipokuwa amekuja na kutokana na hiyo ndio amepata maambukizi. Lakini jambo la kutia moyo ni kwamba baada ya kugundua kwamba yule mgonjwa wa kwanza ana Ebola, hatua zilichukuliwa kuhakikisha wale wote ambao kwa namna moja au nyingine walikutana na yule mgonjwa na kumgusa yule mgonjwa. Wakawekwa katika sehemu maalum ya karantini. Na sababu hiyo ndio namna muhimu ya kuzuia kwamba huu ugonjwa usiweze kuenea”
• Tungali na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO, ambalo leo pia limetoa wito kwa kila nchi duniani kuimarisha hatua za kuzuia watu kuathiriwa vibaya na sumu ya madini ya risasi, kwa lugha ya kiingereza lead, ambayo inakadiriwa kuchangia vifo vya watu zaidi ya milioni 3.5 duniani kila mwaka, huku mamia ya mamilioni ya watoto wakiwa katika hatari kubwa ya kuathirika kwa sababu ubongo na mfumo wao wa fahamu bado vinaendelea kukua. Richard Brown ni Mtaalamu Kiongozi wa Kiufundi na mionzi wa WHO na anasema “Jambo la muhimu sana ni kwamba hatari hizo zinaweza kuzuilika. Watoto wako katika hatari kubwa kwa sababu, kwa bahati mbaya, huingiza mwilini kiasi cha risasi mara nne au tano zaidi kuliko watu wazima kutoka kwenye mazingira au chakula. Na watoto wadogo hasa, kutokana na tabia ya kuweka mikono au vitu vinywani mwao katika mazingira yaliyochafuliwa na risasi, huongeza kiwango cha kukabiliwa na hatari hiyo.”
• Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa licha ya nchi nyingi duniani kuweka malengo ya kulinda bayonuai hatua zinazochukuliwa bado hazitoshi kuzuia kupotea kwa viumbe hai na uharibifu wa mazingira. Akizungumza mjini Yerevan, Armenia, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya hatua za kulinda biyoanuai Guterres amezitaka nchi “kuongeza fedha na uwezo wa nchi zinazoendelea, kutimiza ahadi za misaada ya maendeleo, na kuondoa ruzuku zinazochangia uharibifu wa mazingira.”.
Mwenyeji wako ni Cynthia Akhangwa, karibu!