Opens in a new window
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya stadi kwa vijana tunamulika jinsi gani vijana waliojiendeleza katika stadi ya akili mnemba au wengine wanaita akili unde, kwa kiingereza Artificial Intelligence au AI, wanarahisisha maisha ya jamii. Na tunamuangazia kijana Kalebu Gwalugano kutoka Tanzania, Muasisi na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Neurotech iliyoanzishwa mwaka 2022. Kijana huyu ni Mhandisi wa AI na akiwa Dar Es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa taifa hilo la Afrika Mashariki, amezungumza na mwenzetu Japhael Jambo. Pia tunakuletea Muhtasariw a habari.Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Stadi za Vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema kuwezesha vijana kufikia uwezo wao kamili kunahitaji uwekezaji mkubwa katika elimu na mafunzo jumuishi yenye ubora. Ametambua mchango wa vijana kote duniani kwamba wanaendelea kutoa mchango mkubwa kama wabunifu, viongozi na mawakala wa mabadiliko katika kujenga jamii zenye usawa, ustahimilivu na maendeleo endelevu hata hivyo mabadiliko ambayo dunia inapitia sasa yakichochewa na maendeleo ya teknolojia za kidijitali, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika wa kiuchumi na pengo la usawa yanahitaji vijana kuwa na ujuzi mpya unaowawezesha kushindana na kunufaika na fursa zinazojitokeza.Ingawa mwaka 2025 duniani kiwango cha chanjo kwa watoto kiliongezeka kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, kiwango cha chanjo bado kiko asilimia moja chini ya kiwango cha mwaka 2019, kikiwa kimeendelea kubaki ndani ya kiwango finyu tangu mwaka 2009. Hayo ni kwa mujibu wa makadirio ya kila mwaka ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani, WHO na la kuhudumia watoto, UNICEF kuhusu viwango vya kitaifa vya chanjo.Na ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR inazitaka pande zinazohusika katika vita nchini Sudan, pamoja na serikali na kampuni zinazofanya biashara ya Gum Arabic, gundi inayotokana na aina fulani ya miti ya Acacia kuhakikisha shughuli zao zinaendana na sheria za kimataifa na hazichangii kuendeleza mzozo.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!