Skip to content
Opens in a new window
13 OKTOBA 2026
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina Waswahili wana msemo usemao, Mungu hakupi kilema akakunyima mwendo. Tafsiri yake inaweza kuwa kwamba kila changamoto unayopitia katika Maisha inaweza kuja na fursa nyingine.

Mfano halisi ni wa Maisha ya kijana ambaye utasikia simulizi yake katika mahojiano yafuatayo. Kijana huyu hivi sasa ni mpiga picha za mazingira na ni mwanaharakati mchechemuzi wa kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Anold Kayanda alizungumza na kijana huyu hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York-Marekani wakati wa wiki ya Mjadala Mkuu wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA81.

Pia tunakuletea muhtasari wa habari:

• Leo ni siku ya kimataifa ya kupunguza athari za majanga, Umoja wa Mataifa unapigia chepuo uimarishwaji wa juhudi za kujiandaa kabla ya majanga na kusaidia jamii kujikwamua baada ya dharura, kwa lengo la kulinda maisha, kupunguza watu kulazimika kuhama makazi na kujenga ustahimilivu wa jamii. Akizungumza siku hii Maria Moita Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio na Urejeshaji wa Kibinadamu wa Shirika la Umoja waMataifa la Uhamiaji IOM amesema, “maandalizi ya mapema hupunguza athari mbaya za majanga, huku mipango ya urejeshaji ikisaidia waathiriwa kurejea katika maisha yao kwa usalama na utu.”
• Huko Medellín, nchini Colombia, jamii zinazoishi kando ya mito zimeelimishwa kuwa tahadhari za mapema ni pamoja na kumtambua Jirani yako, kushirikishana taarifa na kuhakikisha kila mtu anajua la kufanya hatari inapoongezeka. Carolina Vásquez, Kiongozi wa Kundi la Kijamii la Tahadhari za Mapema, anasema, “jukumu letu kama jamii ni kuufuatilia mto mara kwa mara na kuangalia mabadiliko yake na kujiandaa kwa tahadhari yoyote. Naye José Rodolfo Sánchez, kutoka Kamati ya Jamii ya La Planta, anasema maandalizi huanzia nyumbani na kuimarishwa kupitia mafunzo, mazoezi na kusaidiana miongoni mwa majirani, akisema “tunafundisha jamii thamani ya kila mtu. Hakuna vinyongo, hakuna wivu. Kuna thamani ya uhai wa kila mtu mwingine.
• Na taarifa mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM imebainisha kuwa safari za kupitia baharini kutoka Afrika Magharibi kuelekea barani Ulaya zikizidi kuwa za hatari zaidi, idadi ya wanaoweka rehani maisha yao kusaka maisha bora barani Ulaya imepungua kwa kiasi kikubwa, asilimia 59. Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope ametahadharisha kuwa “Mara nyingi wahamiaji hubadili njia na kuelekea sehemu nyingine. Ndiyo sababu ni muhimu kuangalia safari nzima, kuanzia wanakoondoka hadi wanakofika.”.
Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!