
About
Hii leo jaridani tunaangazia ujumbe wa António Guterres hii leo huko Addis Ababa nchini Ethiopia, wanawake wanaowasili Ulaya kufuatia ukeketaji wa lazima katika nchi zao, na mafunzo ya kutatua migogoro kwa njia mbadala Zanzibar.Huu ndio mkutano wangu wa mwisho kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema António Guterres, baada ya mkutano wa 10 wa pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa hii leo huko Addis Ababa, Ethiopia, huku akijinasibu kuwa ushirikiano kati ya vyombo hivyo wakati wa kipindi chake cha miaka 10 umekuwa moja ya mifano imara ya ushirikiano thabiti wa kimataifa.Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania, limetoa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa kutatua migogoro kwa njia mbadala (ADR), wasaidizi wa kisheria 126 kutoka kisiwani Pemba, Zanzibar ili kusogeza huduma za kisheria karibu na jamii na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.Wanawake wengi wahamiaji na wakimbizi kutoka Afrika wanaowasili barani Ulaya wakisaka usalama na maisha bora hujikuta wakikabiliwa na majeraha ya kiwewe, changamoto za lugha na kutengwa kijamii. Nchini Ujerumani, shirika lililoanzishwa na wakimbizi, la AfroKids International, linafanya kazi ya kuwapa matumaini na msaada wanawake hao, hususan manusura wa ukeketaji au FGM. Akizungumza na Flora Nducha Idhaa hii kandoni mwa mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70 uliomalizika mwezi uliopita hapa Umoja wa Mataifa, Farina Gorma afisa mkuu wa shirika hilo la kimataifa katika ofisi ya Stuttgart amesema wanawake wengi wanaowasili Ulaya hukumbana na mtihani hasa wa kupata huduma za afya, msaada wa kisheria na usaidizi wa kisaikolojia..Mwenyeji wako ni Anold Kayandai, karibu!