
About
Hii leo jaridani tunaangazia Siku ya Redio Duniani likitupeleka nchini Tanzania kusikia jinsi ambavyo redio inavyochochea maendeleo ya kijamii, nchini Uganda kumsikia mkimbizi kutoka DRC, na katika ukanda wa Gaza ambako redio inaunganisha tena jamii ndani ya vifusi.Leo ni siku ya redio duniani ambayo msingi wake unatokana na kuanzishwa kwa redio ya Umoja wa Mataifa tarehe 13 Februari mwaka 1946 jijini New York, Marekani. Kwa mantiki hiyo ikiwa mwaka huu redio hiyo ya Umoja wa Mataifa inatimiza miaka 80 tumeangazia mchango wa vipingi vyake vilivyokuwa vinarushwa na redio zingine ikiwemo iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) nchini Tanzania wakati huo. Assumpta Massoi amemulika suala hilo.Katika maeneo ya migogoro, duniani redio huwa nguzo ya utulivu na wakati mwingine daraja la kuokoa maisha. Na ndivyo ilivyokuwa kwa mkimbizi Bahati Yohane kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwani kwake, redio haikuwa tu combo cha habari ilikuwa dira ya kuokoa maisha yake.Kabla ya vita vya sasa kuanza katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina lilalokaliwa kimabavu na Israel, Redio ilikuwa chombo muhimu kwa umma na kwa hakika umuhimu wake haujakoma isipokuwa huduma ya matangazo ya redio ndio iliyokuwa imekoma kutokana na vituo vya redio kusambaratishwa kwa makombora, lakini sasa juhudi zinafanyika kuirejesha huduma hiyo muhimu.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!