Skip to content
Opens in a new window
12 OKTOBA 2026
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kumulika juhudi za kukabiliana na upotevu na utupaji wa chakula kupitia teknolojia bora za uhifadhi, usambazaji wa chakula kilichozidi na matumizi ya Akili Mnemba (AI), hatua zinazolenga kuharakisha utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu, (SDG) namba 12.3.

Kupitia mahojiano na Assumpta Massoi wa Idhaa hii katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi, Meneja wa Miradi na Mtaalamu wa Maarifa hiyo, Michael Muratha, amesema kupunguza upotevu wa chakula ni muhimu katika kuimarisha uhakika wa chakula, kulinda mazingira na kuongeza kipato cha wakulima.

Pia tunakuletea muhtasari wa habari:

• Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP na Chuo Kikuu cha Oxford imeonesha kuwa idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa duniani imeongezeka kwa watu milioni 51.5, na kufikia watu bilioni 1.2, kwa mara ya kwanza katika miaka 15. Mkuu wa UNDP, Alexander De Croo, amesema, “Kuongezeka kwa umaskini kunapaswa kuwa kengee ya kuiamsha dunia ichukue hatua.” Amesema watu hao wanakabiliwa na changamoto zinazochocheana, zikiwemo njaa, ukosefu wa elimu, maji safi na umeme. Hata hivyo, De Croo amesisitiza kuwa, “Tunajua kwamba maendeleo yanawezekana,” akizitaka nchi zichukue hatua madhubuti na kushughulikia changamoto hizi kwa pamoja.
• Ukata wa fedha unahatarisha msaada na ulinzi kwa watu milioni 117 waliolazimika kuyahama makazi yao kote duniani limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi UNHCR. Kamishina Mkuu wa UNHCR, Barham Salih, amesema shirika hilo limepokea dola bilioni 3 pekee kati ya dola bilioni 8.5 zinazohitajika mwaka huu. Amesisitiza kuwa, “Kuna tofauti kati ya kufanya mambo mengi kwa rasilimali chache na kuombwa kufanya jambo lisilowezekana,” akibainisha kuwa wafanyakazi 8,000 wamelazimika kuondoka kazini tangu mwaka 2024.
• Na Shirika la Afya la Umoja wa Maataifa Duniani (WHO) limeweka lengo la kuhakikisha kila nchi inagundua na kuelewa vitisho vipya vya kiafya ndani ya saa 24 tangu vinapojitokeza, ifikapo mwaka 2030. Akizindua mkakati huo mpya mjini Berlin, Ujerumani, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema lengo ni kuchukua hatua mapema kabla milipuko haijageuka kuwa majanga makubwa. Akitaka kuwa na “Dunia ambayo kila nchi inaweza kuchukua hatua haraka dhidi ya vitisho vya kiafya kabla havijageuka kuwa majanga makubwa. WHO inasema kufanikisha lengo hilo kutahitaji uwekezaji endelevu na ushirikiano wa kimataifa ili kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na kulinda jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa.
Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!