
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Côte d'Ivoire ambako wakulima wameshuhudia kuimarika taratibu kwa uzalishaji wa kakao baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO kusaidia wakulima nchini humo kurejesha ardhi katika ubora wake na kuongeza uzalishaji kupitia mbinu endelevu za kilimo mseto cha misitu, mazao na mifugo..Afrika imekuwa mstari wa mbele kushinikiza mfumo mpya wa kifedha unaozingatia usawa kwa nchi zinazoendelea. Na leo katika mkutano wa kuangazia mustakbali wa Afrika, Africa Forward huko Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezipongeza nchi za Afrika kwa kuongoza juhudi hizo za mageuzi ya mifumo ya fedha duniani. Kuhusu utajiri wa madini yanayopatikana Afrika kunufaisha nchi nyingine nje ya bara hilo Guterres amesema “Hakuna tena unyonyaji wala uporaji. Watu wa Afrika lazima wanufaike kwanza, na zaidi kutokana na rasilimali za Afrika.”.Taarifa mpya kuhusu virusi vya hanta ni kwamba hadi sasa wagonjwa walioripotiwa ni 11, na watu watatu wamefariki dunia. Kati ya wagonjwa hao, tisa wamethibitishwa kuwa na virusi vya Andes huku wawili wakihesabika kuwa wagonjwa wanaoshukiwa lilesema shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO. WHO pia wameipongeza serikali ya Hispania kwa ushirikiano wake katika mchakato mzima wa kuwaondoa salama na kuwarejesha makwao abiria takriban 150 kutoka nchi 23 waliokuwa katika meli ya kitalii ya MV Hondius ambapo humo ndio mlipuko wa hanta ulipotokoea.ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa hivi karibuni kuhusu Malengo ya Misitu Duniani, Global Forest Goals kwa mwaka 2026 ikieleza bayana kuwa misitu ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuwai, kuimarisha uhakika wa chakula na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu duniani. Nchini Kenya mkazi mmoja ameeleza bayana jinsi wanavyonufaika na msitu asili wa Ngong ulioko takribani kilometa sita kutoka mji mkuu Nairobi.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania anafafanua maana ya neno “Payapaya’’Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!