About
Hii leo tunaangazia miaka 25 baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, elimu na athari za mabadiliko ya tabianchi, na mbinu za kipato za wavuvi na ulinzi wa mazingira nchini Kenya.Miaka 25 baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, yaliyotikisa Marekani na dunia nzima, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaenzi karibu watu elfu tatu waliopoteza maisha, manusura na wahudumu wa huduma ya kwanza waliojitolea kuokoa wengine. Kwa wale waliokuwa New York siku hiyo, kumbukumbu ya mashambulizi hayo bado ni ya hofu, mshikamano na athari ambazo zinaendelea kusikika hadi leo.Zaidi ya wanafunzi milioni 171 duniani sawa na mwanafunzi mmoja kati ya kila kumi wa umri wa kusoma shule walikumbwa na usumbufu wa masomo kutokana na majanga ya tabianchi mwaka 2025 kwa mujibu wa uchambuzi mpya uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.Nchini Kenya, mradi wa kuboresha mbinu za kipato za wavuvi na kulinda mazingira unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kupitia Kamisheni ya Masuala ya Uvuvi kwa Ukanda wa Kusini-Magharibi mwa bahari ya Hindi (SWIOFC) umeanza kuleta nuru kwa jamii za wavuvi kwenye kaunti ya Kwale nchini humo. Kwa sasa kiwango cha uvuvi mathalani dagaa kimeongezeka na kuibua changamoto ndani ya mafanikio.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!