
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina na leo tunakwenda Afrika Mashariki hususan nchini Tanzania katika visiwa vya Zanzibar. Tunamulika jinsi serikali ya Zanzibar kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo nchini humo, UNDP wanaboresha huduma za utalii kwa kutumia Akili Mnemba au AI. Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa kupunguzwa kwa misaada rasmi ya maendeleo tangu Januari 2025 kumesababisha takribani wanawake na wasichana milioni moja duniani kupoteza huduma muhimu katika nchi zilizoathiriwa na migogoro. Ikitolewa leo Geneva, Uswisi na New York, Marekani na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake, UN Women, ripoti hiyo iliyopatiwa jina ‘Zaidi ya Kiwango cha Kuvumilika’ miongoni mwa changamoto ilizozitaja ni pamoja na kuwa asilimia 84 ya mashirika ya wanawake yameripoti kuongezeka kwa mahitaji ya huduma, lakini takribani asilimia 90 ya mahitaji hayawezi tena kuyakidhi na kwamba mashirika mawili kati ya matano yanatarajia kufungwa ndani ya mwaka mmoja kutokana na ukosefu wa fedha.Huko Sudan, nchi inayoumia kwa vita kwa miaka minne sasa, kumetangazwa mlipuko mpya wa ugonjwa wa kipindupindu hali inayozidisha wasiwasi kuhusu usalama wa jamii zilizo hatarini, hususan katika mji wa El-Obeid uliozingirwa, ambako mashambulizi ya kila siku ya ndege zisizo na rubani yanaendelea kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu. Dkt. Shible Sahbani, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) nchini Sudan akizungumza kwa njia ya video na waandishi wa habari leo mjini Geneva, uswisi amesema, “tumerekodi zaidi ya wagonjwa 1,330 wa kipindupindu, huku watu 114 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo. Hii inaonesha kiwango cha vifo miongoni mwa wagonjwa wa kipindupindu cha asilimia 13.7, ambacho ni cha juu sana. Na bila shaka, msimu wa mvua unaotarajiwa utaifanya hali kuwa mbaya zaidi.”Na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuhusu Ufuatiliaji wa Elimu Duniani, umeonesha kuwa misaada ya kimataifa kwa sekta ya elimu imeendelea kupungua na nchi 113 duniani zinatumia fedha nyingi kulipa madeni kuliko pesa wanazoziwekeza kwenye elimu. Matokeo ya utafiti huo yamewekwa wazi leo mbele ya viongozi kutoka nchi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa Mageuzi ya Elimu TES+4 unaofanyika Paris, Ufaransa ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa kwanza wa Mageuzi ya Elimu uliofanyika mwaka 2022 na pia ili kusongesha zaidi ufikiaji wa Lengo namba 4 la Maendeleo Endelevu linalohusu Elimu Bora.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!