
About
Hii leo jaridani tunaangazia washindi wa Tuzo ya UNFPA, harakati za kutokomeza Ebola nchini DRC, na watoto wenye ulemavu nchini Kenya. Profesa Serigne Gueye, daktari bingwa wa mfumo wa njia ya haja ndogo kutoka Senegal na mmoja wa wataalamu mashuhuri duniani wa matibabu ya fistula ya uzazi, amesema kutokomeza tatizo hilo kunategemea kuimarishwa kwa mifumo ya huduma za afya ya uzazi na kuhakikisha kila mwanamke anapata huduma za dharura za uzazi kwa wakati.Wakati mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo ukiendelea kuenea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hatua zimepigwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Uwezo wa kutoa matibabu umeongezeka, linasema Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO na kuwaruhusu ndugu kuwaona jamaa zao kumeongeza utayari wa wagonjwa kujitokeza.Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa juzi Julai 7 imeeleza kuwa ingawa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yameboresha maisha ya mabilioni ya watu duniani, kasi ya maendeleo bado haitoshi kufikia malengo yaliyowekwa ili kufikia mwaka 2030 yawe yametimizwa. Na ingawa Umoja wa Mataifa unaendelea kuhamasisha kuwa hakuna anayepaswa kuachwa nyuma katika maendeleo lakini kundi la watu wenye ulemavu bado linakumbana na changamoto nyingi. Kevin Keitany wa Radio washirika wetu Radio Domus ya nchini Kenya ametembelea moja ya mashirika yanayosaidia watu wenye ulemavu nchini humo ili kuangazia harakati zao za kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!