09 JANUARI 2026
About
Hii leo jaridani tunaangazia uchaguzi mkuu nchini Uganda, elimu kwa watoto nchini Sudan leo ikitimia siku 1000 tangu kuzuka kwa vita nchini humo, na juhudi za wanawake za kuhifadhi misitu huko Narok nchini Kenya.Ikiwa zimebakia siku 6 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Uganda, hii leo Umoja wa Mataifa imetoa ripoti inayobainisha kuwa uchaguzi huo utafanyika katika mazingira yaliyogubikwa na ukandamizaji, vitisho dhidi ya wapinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu, na waandishi wa habari.Leo imetimia siku 1000 tangu kuzuka kwa vita nchini Sudan, vita vinavyohusisha Jeshi la Sudan SAF na Kikosi cha Wanamgambo wa Sudan cha Msaada wa Haraka RSF. Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limesema mtu mmoja kati ya watatu nchini humo ni mkimbizi ndani yanchi yake au amekimbilia nje ya nchi huku Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF likieleza mzozo huo ambao umeendelea kusababisha janga kubwa la kibinadamu unawatesa zaidi wanawake na watoto kwani wanabeba mzigo mkubwa wa madhara ya vita.Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, (UNDP), nchini Kenya, kupitia mradi wa kuhimili tabianchi au Climate Promise Guarantee, limewawezesha wanawake wa jamii ya asili katika Kaunti ya Narok, nchini humo kuongoza juhudi za uhifadhi wa misitu huku wakilinda urithi wao wa kitamaduni na kuboresha maisha ya familia zao.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!