About
Hii leo jaridani tunaangazia ugonjwa unaotokana na virusi vya hantavirus, njaa na afya kwa raia nchini Somalia, na ujumbe wa mshiriki wa mkutano wa CSW70 Hanna Wendot Cheptumo Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Maslahi ya Watoto wa Jamhuri ya Kenya kuhusu ukeketaji.Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika linafuatilia kwa karibu na kutoa msaada unaohitajika kufuatia tukio la afya ya umma kuhusu ugonjwa wa Virusi vya Hanta uliothibitishwa kutokea katika meli ya kitalii iliyosafiri katika Bahari ya Atlantic ambapo mpaka sasa watu watatu wamepoteza maisha.Wanawake na watoto waliokimbia ukame na migogoro nchini Somalia wameonya kuwa wanazidi kutumbukia katika janga la kibinadamu la njaa na mateso huku kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu kukiendelea kuathiri maisha ya watu kote nchini humo. Onyo lao limetolewa wakati mkuu wa masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, akihitimisha ziara yake katika kambi za wakimbizi na vituo vya afya mjini Mogadishu na Baidoa mwishoni mwa wiki.Ukeketaji bado ni changamoto katika maeneo kadhaa duniani na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO hadi mwaka jana kulikuwa na zaidi ya wasichana na wanawake zaidi ya milioni 230 walio hai waliokeketwa katika nchi 30 za Afika, Mashariki ya Kati na Asia. Kupitia mahojiano yaliyofanyika kandoni mwa Mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani, CSW70 jijini New York, Marekani, miezi miwili iliyopita, Hanna Wendot Cheptumo Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Maslahi ya Watoto wa Jamhuri ya Kenya anaeleza hatua zinazochukuliwa na nchi yake kupambana na hali hiyo ya ukeketaji.”Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!