02 DESEMBA 2025
About
Hii leo jaridani tukiendelea kukupa taarifa mbalimbali kuhusu siku 16 za kuhamasisha umma kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, leo tunaelekea Mjini Hoima Magharibi mwa Uganda kusikia hisia za wanawake kuhusu ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni.Watu takribani 100,000 wamekimbia makazi yao kaskazini mwa Msumbiji ndani ya wiki mbili, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR likionya kuwa mashambulizi yanaongezeka na kuyakumba hata maeneo yaliyokuwa salama. Mwakilishi wa UNHCR, Xavier Creach, amesema mgogoro “unazidi kuzorota kwa kasi ya kutisha” huku familia zikikimbia usiku gizani wakati watu wenye silaha wakivamia vijiji vyao. UNHCR inasema linahitaji dola milioni 38.2 kukidhi mahitaji yanayoongezeka.Kaskazini mwa Asia, dhoruba za kitropiki na mvua zisizo za kawaida zimesababisha vifo vya mamia na watu wengi kukimbia makazi yao, imesema WMO. Clare Nullis, msemaji wa shirika hilo, alisema Indonesia, Ufilipino, Sri Lanka, Thailand na Vietnam ndizo zimeathirika zaidi. “Tunahitaji kuzingatia kuwa Asia iko hatarini sana kutokana na mafuriko,” amesema Nullis, akibainisha kuwa dhoruba karibu na Ekweta ni nadra na jamii hazina uzoefu wa kukabiliana nazo. Indonesia pekee, watu 604 wamefariki, 464 hawajulikani walipo, na 2,600 wamejeruhiwa, huku zaidi ya milioni 1.5 wakiathirika na 570,000 wakikimbia makazi yao.Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa leo Desemba      2 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani ILO limeonya kuhusu kuongezeka kwa utumwa wa kisasa wa binadamu, likionesha kuwa watu milioni 10 zaidi walikuwa wakiishi katika kazi za kulazimisha au ndoa za shuruti mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka 2016. Makadirio haya mapya yanaweka idadi ya walioathirika duniani kote kuwa watu milioni 50 huku wanawake na watoto wakiendelea kuwa wenye hatari kubwa zaidi.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali "KOTI LA BABU HALIKOSI CHAWA".Mwenyeji wako ni Sabrina Moshi, karibu!