
About
Hii leo jaridani tunaangazia ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Siku ya UKIMWI Duniani, simulizi wa mwathirika wa ugonjwa huu amabye aliolewa na umri wa miaka 15, na juhudi za UNICEF Wajir nchini Kenya za kuhakikisha ujumuishwaji wa watoto wenye ulemavu darasani.Leo ni Siku ya UKIMWI Duniani na mwaka huu inaadhimishwa kwa onyo kali kuhusu janga hilo pamoja na wito wa kuchukua hatua. Ikibeba kaulimbiu “Kukabili misukosuko, kubadili mwelekeo wa hatua za UKIMWI,” Umoja wa Mataifa unasema dunia ipo katika kipindi cha uamuzi muhimu katika vita dhidi ya VVU.Pooja aliolewa akiwa na umri wa miaka 15, baadaye akiwa mdogo bado akagundua kuwa ana Virusi Vya Ukimwi, VVU, na leo ni Mratibu wa Kitaifa wa Vijana chini ya Muungano wa Kitaifa wa Watu wanaoishi na VVU nchini India (NCPI+), akifanya kazi moja kwa moja na zaidi ya vijana 1,800 kote India. Katika mahojiano yaliyofanywa na Anshu Sharma wa Idhaa ya Kihindi ya Umoja wa Mataifa, Pooja anasimulia safari yake, nafasi ya jamii na familia, na ujumbe wake kwa watu wanaoishi na VVU. Anaposema ART anazungumzia dawa za kufubaza virusi, sawa na ARV lakini katika mkusanyiko wa dawa nyingi kwa pamoja.Katika Kaunti ya Wajir Kaskazini Mashariki mwa Kenya, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Maalum ya Kenya KISE wameanzisha mpango maalum wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu kupata tathmini za kitabibu na kielimu. Mpango huu umeleta matumaini mapya kwa familia nyingi ambazo hapo awali zilikuwa na ugumu wa kupata huduma hizo.Mwenyeji wako ni Sabrina Moshi, karibu!